Kuzimwa nchini Myanmar: Hadithi Mpya Yenye Changamoto za Zamani
26/7/2021 - 4 dakika za kusoma
Imesasishwa: 26/9/2021
Kuhudumia watumiaji milioni 5 nchini Myanmar si jambo dogo
Wakati Intaneti inapozimwa, ndivyo mawasiliano na ulimwengu wote yanavyozimika pia. Tunajua kwamba serikali nyingi hutumia udhibiti wa Intaneti kama njia ya kukandamiza uelewa wa umma, maandamano ya kiraia, na uhamasishaji, na tukio la kuzima Intaneti mara nyingi huwa ni ishara ya mambo mabaya yajayo. Hii inamaanisha habari mbaya zaidi zinanyemelea. Wakati taa za ruta zilipozimika nchini Myanmar, ulimwengu mzima ulibadilika kwa mamilioni ya raia wa Myanmar...
“Mshtuko na kutoamini kabisa” ndivyo kijana mmoja wa Myanmar alivyoelezea hali ilivyokuwa baada ya mapinduzi mnamo Februari. “Nilipoteza mwelekeo,” na pia “kazi yangu”. Hakuwa mtu pekee aliyeshuhudia kiwango hiki cha kuvurugikiwa: karibu raia milioni 2 wa Myanmar walimiminika kwenye mtandao wa Psiphon katika kipindi cha siku chache tu. Idadi hiyo iliongezeka baadaye na kufikia milioni 5 katika miezi michache iliyofuata.
Grafu iliyo hapa chini inaonyesha idadi ya watumiaji wa Psiphon kati ya mwishoni mwa Januari 2021 na mwishoni mwa Julai, 2021. Zingatia ongezeko kubwa la ghafla la idadi ya watumiaji mnamo Februari 3 (likiambatana na mapinduzi) na mnamo Mei 2, likiambatana na kuanza tena kwa huduma za simu za mkononi.

Gharama ya Kurejesha Upatikanaji wa Intaneti ya Kimataifa
Mtandao wa seva unaoweza kuhimili ongezeko kubwa kama hilo la matumizi unahitaji kuwa na miundombinu thabiti na uwezo mkubwa wa akiba kwa ajili ya wakati watu wanapohitaji kupata Intaneti ya kimataifa. Lakini, mambo haya hufanyaje kazi wakati wadhibiti wanapozuia Intaneti?
Wazia Intaneti kama barabara, na watu wanaovinjari kwenye Intaneti kama wanaoendesha magari kwenye njia hizi. Baadhi ya barabara ni za ndani ya jiji wakati nyingine zinaweza kukuunganisha na maeneo mengine ya nchi. Udhibiti unafanana na kuzuia msongamano wa magari kwenye barabara kuu za kitaifa au za ndani. Unaweza kufanywa kwa njia mbalimbali kuanzia kulazimisha mwendo wa polepole hadi kuondoa alama za barabarani zinazoonyesha jinsi ya kuondoka jijini.
Hapo ndipo zana za kupambana na udhibiti kama vile Psiphon zinapoingia kazini na kufungua barabara. Psiphon hutumia mbinu tofauti kuwaunganisha watu na Intaneti ya kimataifa.
Mtandao wa Psiphon huendesha itifaki tisa tofauti zinazowaunganisha watu na kuwasilisha maudhui yaliyodhibitiwa. Itifaki hizi, zinapoendeshwa ndani ya Mtandao wenyewe wa Psiphon, husaidia kusambaza mzigo wa mtandao na kupunguza msongamano wakati watu wanapofikia Intaneti ya Kimataifa, jambo linalomaanisha muunganisho wa kasi zaidi na uzoefu wa kutegemewa zaidi.
Unyumbulifu ambao itifaki hizi maalum za Uhuru wa Intaneti hutoa kwa huduma kama vile Psiphon, hufanya iwezekane kuitikia miito ya watu nchini Myanmar, Belarus au Azerbaijan wakati upatikanaji wa Intaneti unapokuwa na vikwazo, lakini inakuja na gharama halisi; kila baiti inayopita kwenye Mtandao wa Psiphon inavuka mfululizo wa mitandao ya kibiashara, na kila mmoja unatoza bei yake kwa ajili ya seva na miundombinu ya mtandao.
Kusawazisha mahitaji na gharama
Kuhakikisha mtandao uko tayari kusaidia mamilioni ya watumiaji, wakati wowote unapohitajika, bado ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi kwa jumuiya ya Uhuru wa Intaneti katika mapambano yao dhidi ya udhibiti kote ulimwenguni.
Kama inavyokuwa kwa mtoa huduma mwingine yeyote anayepatikana bure, Psiphon haiwezi kudumisha aina hii ya ongezeko kubwa la idadi ya watu lililoonekana nchini Myanmar kwa muda usiojulikana, wala kuhimili ongezeko kadhaa kama hili likitokea kwa wakati mmoja. Hili linasikitisha sana, kwani linaweza kumaanisha kupotea kwa matumaini ya mwisho ya watu wengi ya kupata Intaneti iliyo wazi, wakati ambapo wanaihitaji zaidi.
Hata hivyo, ingawa uhuru wa Intaneti ni haki ya msingi ya binadamu, kwa hakika si wa bure.
Jihusishe
Uhuru wa Intaneti ni haki ya wote, lakini ni wachache tu miongoni mwetu wenye uwezo wa kusaidia watu katika maeneo yanayotekeleza udhibiti ili wapate intaneti iliyo wazi. Kuwa mmoja wao.
Unaweza kufanya nini? Ongeza ufahamu kwa kuzungumzia hali ya intaneti nchini Myanmar, na waalike wengine wazungumzie jambo hilo kwenye mitandao ya kijamii pamoja na marafiki zako na watu wanaojali kuhusu uhuru wa habari. Unaweza pia kusaidia moja kwa moja zana kama Psiphon zinazosaidia watu wenye uhitaji. Jiunge na usajili wa Psiphon ikiwa hauko nchini Myanmar. Kuonyesha msaada wako kwa kila mtu aliyenyimwa haki yake ya kupata habari kwenye intaneti kutamaanisha mengi kwao, na kunamaanisha mengi kwa watu wanaofanya wawezavyo kuleta nuru katika giza la udhibiti.