Heri ya 2017 kwa Watumiaji wa Psiphon!

2/1/2017 - 2 dakika za kusoma

Imesasishwa: 22/1/2025


2016 ulikuwa mwaka wenye matukio mengi, ukiwa na habari tele za ulimwengu za kufahamishwa kuzihusu. Wakati ufikiaji wa Intaneti na hivyo habari ulimwenguni kote ukiongezeka, udhibiti wa kila aina ukiwemo uzuizi wa tovuti nao pia ulipanda.


Hapa Psiphon pia tumeona watumiaji wengi zaidi wa programu yetu kuliko wakati mwingine wowote, na ingawa hii inaenda sambamba na kuongezeka kwa vizuizi vya habari kwenye intaneti, tunafurahi kuweza kuwasaidia watu kuvikwepa.


Ripoti ya kila mwaka ya Freedom House kuhusu Uhuru wa Intaneti ilibainisha kupungua kwa uhuru huo kwa mwaka wa sita mfululizo, na iligundua kuwa theluthi mbili ya watumiaji wa Intaneti ulimwenguni kote wanaishi katika nchi ambazo kukosoa serikali, jeshi au ufalme hupelekea udhibiti. Uchunguzi wao mwingine mkuu ulikuwa kwamba serikali zinazidi kulenga programu za kutuma ujumbe.


Hili linaendana na baadhi ya mambo tuliyoyaona kwenye mtandao wetu mwaka huu. Kwa mfano mnamo Januari huduma za VoIP zilizuiliwa nchini Morocco, zikiwakera watumiaji wa huduma maarufu za kupiga simu bila malipo kama vile Viber, Whatsapp, Skype na Facetime. Kwa muda wa mwezi mzima wa marufuku hiyo, tuliona trafiki yetu ya Morocco ikiongezeka mara tatu katika wiki ya kwanza na kisha kuongezeka maradufu kila wiki baada ya hapo. Kisha mwezi Mei jaji wa Brazili aliamuru uzuizi wa Whatsapp, si kwa mara ya kwanza. Tena tuliona trafiki kutoka nchini humo ikiongezeka mara tatu, safari hii ndani ya saa 24.


Uchaguzi wa kitaifa ni chanzo kingine kikuu cha udhibiti, na tumeona watu wakigeukia Psiphon wakati serikali zao zinapozuia mitandao ya kijamii au tovuti za upinzani, kwa mfano mnamo Agosti nchini Gabon. Mwenendo mwingine ambao tumeuona mwaka huu ni kuzimwa kabisa kwa intaneti katika baadhi ya nchi wakati wa matukio ya misukosuko - jambo ambalo hata Psiphon haiwezi kulifanyia chochote.


Matumaini yetu ni kwamba mnamo 2017 tunaweza kuwasaidia watu ulimwenguni kote kuwasiliana na kupata habari bila vikwazo. Heri ya Mwaka Mpya kwa marafiki zetu wote na tunawatakia 2017 salama, yenye furaha na huru!
Habari za Kampuni

Soma inayofuata